Boban, Okwi kwenda Bondeni

Haruna Moshi ‘Boban’
Emmanuel Okwi.
UWEZO mkubwa waliouonyesha viungo wawili washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi na Haruna Moshi ‘Boban’, umewapa ulaji wa kucheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini.
Boban na Okwi, raia wa Uganda, wamezivutia timu mbili kubwa za Afrika Kusini, Kaizer Chiefs na Jomo Cosmos na kama mambo yataenda vizuri, huenda wakafunga safari kwenda kufanya majaribio nchini humo, hivi karibuni.
Akizungumza na Championi Ijumaa, jana, akiwa Johannesburg, Afrika Kusini, wakala maarufu wa kuuza wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Ivica Stankovic, alisema Boban na Okwi wanaonekana ni lulu nchini humo.
“Tupo katika hatua za mwisho, ninazungumza na Cosmos na Chiefs. Wanawataka wachezaji hao kwa ajili ya majaribio, ikiwezekana wanaweza kuja na kusajiliwa moja kwa moja kwa kuwa Okwi tayari alikuwa hapa na akafanikiwa.
“Hofu yetu ni kitu kimoja, suala la nidhamu na kampuni yangu (Sierra Agency) inahitaji wachezaji ambao watafanya vizuri ili wasiharibu jina kwa timu tuliyoshirikiana nayo,” alisema.
“Tumefanya mazungumzo na Simba, tunajaribu kuangalia uwezekano. Wachezaji wanaotakiwa hapa ni wanne pamoja na beki mmoja na mshambuliaji wa kati. Tayari tumeangalia wachezaji wawili kutoka DRC, mmoja kutoka Zimbabwe, wengine Tanzania na Uganda.
“Kama tukiwa na makubaliano mazuri na Simba, basi tutawapa nafasi ya kwanza wao waje huku. Ikishindikana tutaangalia upande mwingine kwa kuwa hii ni biashara.”
Kwa upande wa Simba, msemaji wake, Ezekiel Kamwaga, alisema bado hawajapokea maombi yoyote kutoka katika klabu hizo za Afrika Kusini wala Sierra Agency.
“Labda mambo yapo njiani au wanajiandaa kuwasiliana nasi, bado sina taarifa hizo na kama zikija basi mara moja tutawapa taarifa,” alisema Kamwaga.
Mwaka jana, Okwi alifanya majaribio Kaizer Chiefs na kufuzu, lakini akachukua uamuzi wa kurejea nchini kuendelea kuichezea Simba kwa madai kuwa hajafurahishwa na mfumo wa maisha ya Afrika Kusini.
Wawili hao wamekuwa wakionyesha kiwango cha juu na kuwasaidia Simba kung’ara karibu kila mechi wanayocheza.

Leave a Reply